Ujumbe kutoka kwa Balozi

2026/9/30

 
Mwezi Mei mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje Motegi alizuru Kenya. Katika hafla maalum ya mhadhara jijini Nairobi, iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Global Centre for Policy and Strategy (GLOCEPS) na Ubalozi wa Japani, alitoa hotuba kuhusu dhana mpya ya “Indo-Pasifiki Huru na Wazi” (FOIP), iliyorekebishwa hivi karibuni, akilenga bara zima la Afrika. Katika hotuba hiyo, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa unaozingatia uwezo wa nchi kujitegemea na ustahimilivu, ili kuhakikisha kuwa ushirikiano huo unachangia ipasavyo utulivu na ustawi katika eneo la Indo-Pasifiki, licha ya misukosuko ya sasa ya siasa za kijiografia. Akifuata mfano wa  hayati Waziri Mkuu Abe, ambaye alipendekeza kwa mara ya kwanza dhana ya awali ya FOIP hapa Nairobi mwaka 2016, Waziri Motegi alisisitiza kuwa Afrika ni mshirika muhimu wa Japani katika kutekeleza kwa pamoja FOIP mpya. Aidha, katika mazungumzo yake na Rais Ruto na mkutano wake na Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, alijadili kwa kina mustakabali wa ushirikiano wa nchi mbili kati ya Japani na Kenya, kwa mtazamo mpana. Mazungumzo hayo ya ngazi ya juu yalikuwa na manufaa makubwa.

Mwezi huu wa Septemba, Mtukufu wa Kifalme Binti Takamado alizuru Kenya. Akiwa Rais wa Heshima wa BirdLife International, shirika linalohimiza uhifadhi wa ndege, alihudhuria Mkutano wa Washirika wa Kimataifa wa shirika hilo. Alihimiza washirika wa BirdLife duniani kuunganisha azma yao, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika uhifadhi wa ndege, kwa kuwa ndege hawatambui mipaka ya kitaifa. Alitoa hotuba katika makao makuu ya UNEP, yaliyoko katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi (UNON). Katika hotuba hiyo, Binti Takamado alisisitiza umuhimu wa kudumisha mazingira yanayowawezesha watu na ndege kuishi kwa maelewano, ili maisha ya binadamu yawe endelevu. Alieleza kuwa, hata tunapokabili masuala mapana ya mazingira, yakiwemo mabadiliko ya tabianchi, maisha endelevu ya binadamu yanategemea kuishi kwa maelewano na mazingira asilia. Aidha, alishiriki katika shughuli mbalimbali za kuendeleza uhusiano kati ya Japani na Kenya, na kati ya Japani na Umoja wa Mataifa. Shughuli hizo zilijumuisha kumtembelea Rais Ruto, kubadilishana maoni na wawakilishi wa taasisi kadhaa zinazohusika na upandaji miti, kuzungumza na Wajapani wanaoishi Kenya, na kuzungumza na Wakenya wanaoshiriki katika kuimarisha uhusiano na Japani.

Ziara hizi mbili za ngazi ya juu zilifuatia ziara mbili za Rais Ruto nchini Japani, zilizofanyika katika miaka miwili mfululizo, 2024 na 2025. Nimefurahishwa sana na ziara hizo, kwa kuwa zinaonyesha kuwa uhusiano wa karibu kati ya nchi zetu mbili unaimarishwa kupitia watu wa nchi hizi mbili kutembeleana. Kwa Waziri Motegi, hii ilikuwa ziara yake ya nne nchini Kenya, na ya pili akiwa Waziri wa Mambo ya Nje. Kwa Binti Takamado, hii ilikuwa ziara yake ya tatu nchini Kenya, na ya pili akiwa Binti wa Kifalme. Idadi hizi zinaonyesha mapenzi yao ya pekee kwa Kenya na zinaeleza kwa ufupi umuhimu wa ziara zao. Mfululizo wa ziara za pande zote, ulioanza na ziara ya Waziri Mkuu Kishida nchini Kenya mwaka 2023 na kuendelea kila mwaka bila kukatika hadi sasa, umeimarisha uhusiano wa nchi zetu mbili na kuupa msukumo zaidi.

Pia ni muhimu kuwa Waziri Motegi na Binti Takamado wote walichagua Kenya kuwa jukwaa la kufikisha ujumbe wao kwa bara zima la Afrika na kwa dunia nzima. Hili linaonyesha kiwango cha imani na matarajio ya Japani kwa Kenya kama mshirika wake katika medani ya kimataifa.

Sasa kwa kuwa moyo wa ushirikiano kati ya Japani na Kenya umethibitishwa tena na kuimarishwa katika ngazi ya juu, jukumu letu ni kuugeuza moyo huo kuwa matokeo halisi. Ningependa kuendelea kushirikiana nanyi, bega kwa bega, katika kutekeleza jukumu hili. Natazamia kwa hamu  kwa hilo.

 
30th Septemba, 2026
MATSUURA Hiroshi
Balozi wa Kipekee na Mwenye Mamlaka Kamili wa Japani

Recommended Information